Buriani Kamaradi
Ndugu yangu
Rafiki yangu
Kamaradi Chachage:
Nani kasema umetuacha?
Eti umefariki!
Kwani mwili ndiyo maisha?
Maisha ni fikra.
Maisha ni vitendo.
Maisha ni ubinadamu.
Fikra zako,
Vitendo vyako,
Ubinadamu wako,
Utadumu.
Leo, kesho, keshokutwa na milele.
Vitendo vyako tutavienzi,
Ubinadamu wako tutauiga,
Fikra zako tutazieneza.
Msomi wa afrika,
Mtetezi wa wanyonge,
Mshabiki wa fikra za kitabaka,
Tabaka la wavujajasho.
Nimetumwa.
Nimetumwa na wasomi wenzako wa afrika kupitia codesria nikuletee salaamu zao.
Wameniambia, nikuage.
Nimekataa.
Sikuagi.
Nitakusindikiza tu.
(Follow link to view the complete poem)
Buriani Kamaradi [Issa Shivji, 12 Julai 2006]
Ndugu yangu
Rafiki yangu
Kamaradi Chachage:
Nani kasema umetuacha?
Eti umefariki!
Kwani mwili ndiyo maisha?
Maisha ni fikra.
Maisha ni vitendo.
Maisha ni ubinadamu.
Fikra zako,
Vitendo vyako,
Ubinadamu wako,
Utadumu.
Leo, kesho, keshokutwa na milele.
Vitendo vyako tutavienzi,
Ubinadamu wako tutauiga,
Fikra zako tutazieneza.
Msomi wa afrika,
Mtetezi wa wanyonge,
Mshabiki wa fikra za kitabaka,
Tabaka la wavujajasho.
Nimetumwa.
Nimetumwa na wasomi wenzako wa afrika kupitia CODESRIA nikuletee salaamu zao.
Wameniambia, nikuage.
Nimekataa.
Sikuagi.
Nitakusindikiza tu.
Uwaone wazee wako,
Majirani zako,
Watu wema wa njombe.
Uchanganyike na viumbe wa ardhi na bahari,
Viumbe visivyo na ubaguzi,
Mipaka,
Unyonyaji,
Ukandamizaji.
Uwashawishi, wafundishe wanadamu maana ya ukombozi. kama ulivyokuwa Unatufundisha sisi daima.
‘ewe Isssa, kwani, Shivji siyo mwana wa adamu?’,
Ukanitania,
Ukichota kutoka hazina ya ucheshi wako bila uchoyo.
‘umejipachikia majina haya yote ya miungu!
Mlimbikazi, we issa!’
‘mungu wa waislamu na mungu wa wakristo,
Mungu wa wahindu na mungu wa wasambaa.
Unataka wapigane?
Wachinjane.
Eti moja ni –a,
Mwingine ni –ji!’
‘futilieni mbali ushenzi wenu wa kubaguabagua!’, ukakasirika.
‘unganeni kujikomboa’, umetusihi,
‘kutoka kwa makucha ya ubeberu na ubepari, unyonge na udhalilishaji.’
Buriani ndugu yangu,
Buriani rafiki yangu,
Buriani kamaradi chachage.
Ufikesalama.
Upumzike na viumbe visivyonyumbishwa na vituko vya wanaadamu.
Nakuahidi.
Nitaufikisha ujumbe wa maisha yako.
Kwa wanaudasa,
Kwa wanaCodersia.
Kwa wana wa Tanzania,
Kwa wana wa afrika………………….buriani………..