Printer-friendly versionSend by emailPDF version
Kiswahili translation available

KASI ya msukumo kuelekea kwenye dunia ya utandawazi ambayo imejionyesha katika kipindi cha muwongo mmoja na nusu uliopita kwa hakika imebadili mwenendo wa historia ya dunia. Msukumo na mbinu mbalimbali zinazotumika kuweka shinikizo la kuimarishwa kwa sera za utandawazi vimeibua pamoja na mambo mengine, namna mbalimbali za vitisho kwa watu wa kada zote za watu maskini duniani. Hofu hiyo inatokana na ukweli kuwa pamoja na athari zingine utandawazi unaelekea kudhoofisha hata huduma muhimu kwa maendeleo ya jamii, hasa sekta za afya na elimu. (With grateful thanks to Lugano Uli Mbwina from Tanzania for the translation.)

Athari za utandawazi katika jamii ya Afrika

Na Adebayo Olukoshi

KASI ya msukumo kuelekea kwenye dunia ya utandawazi ambayo imejionyesha katika kipindi cha muwongo mmoja na nusu uliopita kwa hakika imebadili mwenendo wa historia ya dunia.

Msukumo na mbinu mbalimbali zinazotumika kuweka shinikizo la kuimarishwa kwa sera za utandawazi vimeibua pamoja na mambo mengine, namna mbalimbali za vitisho kwa watu wa kada zote za watu maskini duniani. Hofu hiyo inatokana na ukweli kuwa pamoja na athari zingine utandawazi unaelekea kudhoofisha hata huduma muhimu kwa maendeleo ya jamii, hasa sekta za afya na elimu.

Ingawa utandawazi kwa namna ya kificho unaonekana kama ndiyo sera kuu ya kuchochea maendeleo, utekelezaji wa sera hiyo umeandamana na ubaguzi mkubwa katika nyanja za uchumi kati ya mataifa na hata baina ya watu wa taifa moja.

Ni dhahiri kuwa katika sera hii ya utandawazi wanaofaidika ni kikundi kidogo sana cha watu na ambacho kadri utandawazi unavyokua ndivyo kinavyozidi kuwa kidogo zaidi na na kujiimarisha zaidi kwa kuchuja na kuwatupa mbali hata watu waliokuwa katika ile kada ya kati ya wana maendeleao. Kada hii pia kutokana na sera za utandawazi inajikuta ikiogelea katika kada ya chini iliyogubikwa na lindi la umaskini hohehahe.

Kuna hoja kadhaa zinaelezea ni kwa nini sera ya utandawazi haiendani na manufaa au mafao kwa jamii badala yake wanaofaidika ni watu wachache walioshika mpini wa kisu cha uchumi.

Wataalam wanasema hata mafanikio ambayo hapo awali yaliweza kupatikana kabla ya mfumo huu, sasa yameanza kumong’onyoka kutokana na nguvu ya utandawazi.

Utandawazi umeshindwa kukuza uchumi wa dunia kwa ujumla badala yake kuimarisha uchumi wa nchi ambazo tayari ni tajiri kwa sababu wawekezaji wa kimataifa wenye mitaji mikubwa wamejiwekea mikakati ya muda mfupi ya kujilimbikiza mali kwa kutumia sera ya utandawazi bila hata kujali maafa kwa mamilioni ya wavuja jasho maskini walioko sehemu mbalimbali duniani.

Kwa upande wa Afrika sera ya utandawazi inaizidishia mazonge kwani hata sera ya ubinafsishaji tu, ambayo ndiyo maandalizi ya utandawazi wenyewe tayari imesababisha mtafaruku kiuchumi na kupanua mwanya kati ya matajiri na maskini.

Ndiyo maana, iwapo tunataka kujadili mstakabali wa utandawazi ni vema kuanza kuijadili hofu inayoletwa na sera hiyo kwa njia ya ubinafsishaji unaoendela katika Afrika. Mabadiliko hayo yamesababisha kukosekana kwa haki na badala yake kukithiri kwa uonevu kuwezesha wenye nguvu za kiuchumi kuwapoka hata kidogo walicho nacho watu maskini.

Afrika yageuka koloni mamboleo

Dola, iwe katika nchi inayoendelea au nchi iliyoendelea ndiyo chombo kikuu kinachosimamia maendeleo na ustawi wa ya jamii ya dola hiyo.

Nguvu za dola zilijionyesha kwa wazi zaidi mara baada ya Vita Kuu ya Pili ambapo kulijitokeza aina mbalimbali za mihemuko ya maisha na hivyo kutakiwa kuwa na dola za kusimamia ustawi wa jamii hizo kutokana na maafa ya vita, hasa nchi za Ulaya ambako kuliathirika zaidi.

Kipindi hicho ndicho pia ambacho ukoloni ulikuwa ukifanya juhudi za maksudi kujaribu kuwekeza mitaji katika miundombinu zikiwemo barabara, viwanda na kupanuka kwa sekta za afya na elimu kwa malengo ya “maendeleo.”

Hata hivyo, halikuwa jambo la kushangaza baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika kujikuta zikikabiliwa na majukumu mengi ya huduma za jamii, jambo ambalo pia lilitumika huko nyuma wakati wa kupigania uhuru kama fimbo dhidi ya ukoloni.

Kwa hiyo majukumu mapya ya dola za Kiafrika baada ya uhuru yalikuwa pia kuongeza huduma za afya na elimu na kuongeza uwigo wa ajira na pia kuboresha lishe kwa wananchi, jambo ambalo dola nyingi zilifanikisha kwa viwango vya kuridhisha

Mafanikio hayo yalijitokeza katika kipindi cha 1980, ambapo hali ya maisha ya jamii nyingi za Afrika zilionekana kuwa na maisha bora zaidi na kiwango cha maisha kikaonekana kukua zaidi na hata vifo vya watoto wachanga vikaonyesha kupungua.

Matokeo haya hata hivyo yalitokana na sera za serikali mpya ambazo zilianzishwa kipindi cha 1960 na 1970 huku uchumi ukikua kwa kiwango cha asilima tano hadi saba, kama ilivyokuwa katika nchi ya Cote d’Ivioire na Kenya ambako uchumi ulikua kufikia wastani wa asilimia tisa.

Enzi za Mtafaruku wa Uchumi

Sera mpya za Shirika ya Fedha Duniani (IMF na Benki ya Dunia (WB) iligeuza mafanikio ya mfumo huo na kutagaza ibada za sera za kurekebisha uchumi ambazo kwa namna moja zilikuwa zikionyesha kuwa chanzo cha matatizo ya uchumi wa Afrika ni serikali za Kiafrika.

Mtafaruku wa uchumi wa Afrika kwa hiyo ulichukua nafasi ya mafanikio ya miaka ya 1980s na kuanzisha lawama dhidi ya mifumo ya uchumi ya dola mpya baada kupata uhuru toka kwa wakoloni wa kizungu.

Baadhi ya serikali hizo kwa hiyo hazikuwa na jinsi nyingine isipokuwa kujaribu kuokoa uchumi wa nchi zao kwa kupunguza mafungu yake katika huduma za jamii.

Menejimenti na usimamizi wa mikakati ya marekebisho ya uchumi iliyopendekezwa na IMF na Benki ya Dunia ilizingatia zaidi mfumo wa uchumi huria duniani ambao kwa ujumla unahimiza dola kutojihusisha na usimamizi wa masuala ya uchumi na maendeleo ya jamii.

Sera hii inaelekeza kuachia “huru” nguvu za soko huria kwa kuzingatia “nguvu za masoko”, kuzuia mfumuko wa bei na kuhimiza watu binafsi kushika uendeshaji wa sekta hiyo.

Kwa sera hii, hata vivutio ambavyo vingetolewa kwa watendaji kazi wake viliondolewa badala yake jukumu hilo kuhamishiwa kwa katika soko huria na wakati huo huo kusababisha kuhama kwa wataalam wazalendo kutoka katika eneo la kutoa huduma za jamii kwenda kwenye na eneo la “nguvu za soko huru”.

Mipango ya serikali za kizalendo kuhusu huduma za jamii baadhi yake ili kuwa na matatizo katika utekelezaji, lakini pia ni kweli kuwa ilikuwa mipango yenye malengo mazuri na yaliyo kuwa wazi yaani, kuboresha maisha ya jamii.

Lakini baada ya kuanza kwa marekebisho ya uchumi chini ya miongozo ya IMF na Benki ya Dunia mwelekeo wa mipango hiyo ukaparaganika na nafasi yake kuchukuliwa na watendaji toka sekta binfasi kwa ajili ya kushika soko lililokuwa la vyombo dola.

Kuporomoka kwa huduma za jamii, hasa afya kwa nchi nyingi za Afrika kulikuja kwa kasi ya kutisha baada ya dola kujiondoa, baadhi ya magonjwa ambayo hapo awali yaliweza kudhibitiwa yalirejea. Wastani wa kiwango cha maisha uliokuwa unapanda ukaanza kushuka na vifo miongoni mwa watoto wachana vikaanza kuongoezeka.

Vilio vya malalamiko ili kurekebisha mparaganyiko huo wa uchumi ili kuwepo kwa mfumo mwenye sura ya kibinadamu vilisababisha marekebisho kadhaa. Lakini pia marekebisho haya ambayo yalilenga kuinusuru jamii kutokana na ukali mfumo huu mpya wa maisha hayakusaidia kitu.

Ni kutokana na kuingia kwa Ukimwi, ugonjwa mpya ndipo jumuiya ya kimataifa na watunga sera wake walipogundua kuwa sera za huduma za jamii haziwezi kufanya kazi mbele ya ugonjwa huu usio na dawa.

Kutoka Marekebisho ya Uchumi kulekea Dola ya Kijamii:

Somo kubwa la msingi ambalo tunalipata katika Afrika kutokana na kushindwa kwa sera hizo za marekebisho ya uchumi katika nchi maskini ni kuanzishwa miaka miwili iliyopita kwa sera ya nyongeza ya Mkakati wa Kupunguza Umaskini ((PRSPs) ambayo pia haionyeshi kama inaweza kutoa changamoto la kutosha kukuza uchumi barani Afrika.

Kwa sera yoyote ya uchumi kufanyakazi ni lazima iundwe katika misingi ya kuhusisha jamii ya watakayonufaika nayo na siyo jambo amabalo linaletwa na kupandikizwa toka nje.

Kwa hiyo tunapokazia kuwepo kwa mfumo wa uchumi ambao unakuzwa na dola ndani ya jamii ina maana kuwa wanajamii wenyewe wanatakiwa kushiriki kukuza ichumi wao badala ya kuletewa mikakati ya uchumi toka nje ambayo haiwezi kutekelezeka hapa Afrika.

Kwa hiyo ili kuondokana na mfumo wa uchumi uliopandikizwa, nchi za Afrika na jamii za watu wake wanatakiwa kujitafakari na kuanza kuunda mikakati yake ya uchumi inayozingatia kushirikisha watu wake au kwa maelezo rahisi zaidi uchumi wenye demokrasia ndani. Ni kwa kufanya hivyo bara la Afrika litajenga uchumi madhubuti na endelevu.

* Profesa Adebayo Olukoshi wa International Economic Relations na Katibu Mtendaji wa African Council for the Development of Social Science Research in Africa (CODESRIA), taasisi yenye makao yake makuu Dakar, Senegal.
* Makala hii inatokana na hotuba yake kwenye mkutano wa Haki ya Huduma za Afya, Durban, Afrika Kusini Juni 8 hadi 9 2004.